SEHEMU YA KWANZA: MASOMO
Aprili 27, 2 025.
Somo la Kwanza
Mdo 5:1 2-1 6
Kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani; na katika wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha; walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake; hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao. Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa.
Wimbo wa Katikati
Zab 1 1 8:2-4,1 3-1 5 25-27
Israeli na aseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
Mlango wa Haruni na waseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
Wamchao Bwana na waseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Ulinisukuma sana ili nianguke;
Lakini Bwana akanisaidia.
Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu,
Naye amekuwa wokovu wangu.
Sauti ya furaha na wokovu Imo hemani mwao wenye haki;
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Ee Bwana, utuokoe, twakusihi;
Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi.
Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana;
Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana.
Bwana ndiye aliye Mungu,
Naye ndiye aliyetupa nuru.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Somo la Pili
Ufu 1 :9-1 1 a, 1 2-1 3, 1 7-1 9
Mimi Yohane, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu. Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu, ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu; na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini. Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu. Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo.
Shangilio
Yn 2 0:29
Aleluya, aleluya
Yesu akamwambia, Wewe kwa kuwa umeniona, umesadiki; Wa heri wale wasioniona, wakasadiki.
Aleluya
Somo la Injili
Yn 2 0:1 9-31
Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.
Walakini mmoja wa wale Thenashara, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. Basi wanafunzi wengine wakamwambia, Tumemwona Bwana. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo. Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu. Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye. Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu! Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki. Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.
SEHEMU YA PILI: TAFAKARI
HURUMA YA MUNGU IDHIHIRIKE KATIKA MAISHA YETU
Na, Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
Siku ya Mwisho huwa ndio siku kubwa ya sikukuu (Yn 7:37-38). Mara nyingi tunaita siku ya kilele. Katika sikukuu ya wayahudi ya vibanda, iliyochukua siku nane, siku ile ya Mwisho ilikuwa sikukuu kubwa. Hii ndio chimbuko la Dominika ya Huruma ya Mungu aliyovuviwa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II. Kwamba siku zote nane tokea Dominika ya Pasaka tumekuwa tukiadhimisha sherehe ya Pasaka kwa uzito ule ule kwa siku nane, octave kwa kilatini. Hivyo siku hiyo ya mwisho tunajipatia kitu kikubwa zaida ambacho ni Huruma ya Mungu.
Dominika ya Huruma Ya Mungu ilitangazwa rasmi na Papa Yohane Paulo wa II, mwaka 2 0 0 0 wakati wa kutangazwa kuwa Mtakatifu Sr. Faustina Kowalska. Tunaimba na mzaburi 1 1 8:1 , wakati wa octava ya Pasaka kwamba “mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za mileleâ€. Kwa kuwa katika midomo ya Kristo mfufuka tumepokea ujumbe mkubwa wa Huruma ya Mungu na imekabidhiwa katika huduma ya mitume kwenye chumba cha juu, walipotokewa na Yesu Mfufuka (Yn 2 0:21 -23).
Amani iwe kwenu
Katika somo la Injili tunathibitishiwa Huruma ya Mungu katika maneno ya Yesu “Amani iwe kwenuâ€. Maneno hayo yanatokea kwa msisitizo mara tatu. Maneno hayo yamebeba a) Furaha, b) Msamaha c) Faraja. Huruma ya Mungu huleta furaha tunapojua kwamba tumesamehewa bure, freely forgiven. Mitume walikuwa na woga, wasiwasi na mashaka wakajifungia ndani. Ukiachilia hofu ya Wayahudi lakini pia wamekata tamaa, waliomwomba wakae mkono wake wa kulia na kushoto, amezikwa. Yesu anapowatokea wanajawa na furaha kumwona tena Bwana.
Pia wanajawa na furaha zaidi kwa maneno ya Yesu, “Amani iwe kwenu†kwani wasiwasi wao ulikuwa ni kwamba atawauliza mbona mlikimbia nilipokamatwa, Petro mbona ulinikana, mbona mliniacha wakati wa mateso, lakini Yesu anawajalia msamaha kwa kuwajalia amani. Salamu hii inawatakasa kwa msamaha wasiostahili. Hivyo Kristo mfufuka anawajalia Huruma yake na wanafarijika.
Hiyo ndio furaha tunayopata kwa Yesu tunaposamehewa naye. Tunapojihisi hatupokei tena msamaha, tumefungiwa huruma yake, tumekata tamaa, tunapokosa matumaini kwa sababu ya udhaifu wetu na dhambi zetu, lakini Yesu anatuambia nenda kwa amani dhambi zako zimesamehewa. Furaha, Msamaha na faraja tunayoipata ndiyo Huruma yenyewe ya Mungu.
…Wowote Mtakaowaondolea dhambi wameondolewa;…
Yesu aliona furaha, msamaha na faraja hiyo isiishie tu kwa mitume bali kwa kanisa na ulimwengu mzima. Hivyo Yesu baada ya kuwapa amani, aliwavuvia Roho Mtakatifu na kuwapa mamlaka ya kuwa vyombo vya Huruma ya Mungu kwa njia ya sakramenti ya Kitubio. Mungu anawafanya mitume na waandamizi wao, maaskofu na mapadre kuwa chaneli ya Huruma yake. Pamoja na hayo, kama wabatizwa wote kwa kumpokea Roho Mtakatifu kwa matendo na maneno mema tunakuwa vyombo vya Huruma ya Mungu. Maana yake ni kwamba Mungu amelifanya kanisa kuwa chombo na alama ya upatanisho kwa Huruma ya Mungu.
Hivyo tunapaswa kujiuliza, Je? tunaikimbilia hiyo huruma ya Mungu katika sakramenti ya Kitubio? na Je? tumekuwa chombo cha Huruma ya Mungu kwa wengine? Tukiwa majumbani kwetu? katika familia zetu? makazini? Katika Jumuiya zetu? na popote tunapokuwa? Au tumekuwa chanzo cha watu kukosa furaha, msamaha na faraja?
Ingawa Thomaso alikuwa na mashaka Yesu hakumhukumu, bali alimruhusu ashike na aone inapobubujika Huruma ya Mungu katika ubavu wake. Damu na Maji zinazowakilishwa na miale miwili kutoka ubavu wa Yesu, unaonyesha Huruma ya Mungu kupitia sadaka ya Yesu msalabani kunakozaliwa sakwamenti za kanisa, hasa Ekaristi Takatifu adhimisho la sadaka ya Yesu Msalabani. Thomaso anatufundisha pia wakati wa mashaka, kukata tamaa, kutokuamini, tuikimbilie Huruma ya Mungu katika sakramenti za kanisa, tuguse na tuone, nasi tuseme “Bwana wangu na Mungu wanguâ€. Madonda yake hushinda mashaka yetu, kutokuamini kwetu, majaribu yetu, na zaidi hushinda dhambi.
Yohane anatuambia katika ufunuo, Huruma ya Mungu inaonekana katika vazi la Yesu aliye mfano wa mwanadamu. Naye Yohane anaanguka na kumsujudia kwani alikuwa amekufa na sasa yu hai hata milele na milele. Hivyo katika yeye aliyefufuka tunapokea Huruma ya Mungu. na mwito kwetu sio tu kuipokea Huruma yake bali kuishuhudia kwa wengine kwa kuwasaidia wanaoteseka, kuwa amani kwao wenye mashaka na wasio na amani, kuwa watu wa kusikiliza na zaidi kuleta faraja, furaha na msamaha kwa wengine.
{“Man is called not only to receive and experience the mercy of God, but also called to practice mercy toward others†(Mt 5:7) “Blessed are the merciful for they shall receive mercyâ€}
……………..………..……… Bwana amefufuka kweli Alleluia!……………………………….