"Njoni Mfungue Kinywa"

SEHEMU YA KWANZA: MASOMO
04 Mei, 2 025

Somo la Kwanza
Mdo 5:27b-32, 4 0b-41
Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio. Nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao. Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo.

Wimbo wa Katikati
Zab 3 0: 1 , 3, 5, 1 0-1 2
Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua,
Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
Umeniinua nafsi yangu,
Ee Bwana, kutoka kuzimu.
Umenihuisha na kunitoa
Miongoni mwao washukao shimoni.
(K) Ee Bwana, Mungu wangu, Nalikulilia ukaniponya.

Mwimbieni Bwana zaburi, Enyi watauwa wake.
Na kufanya shukrani. Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.

Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,
Katika radhi yake mna uhai.
Huenda kilio huja kukaa usiku,
Lakini asubuhi huwa furaha.
(K) Ee Bwana, Mungu wangu, Nalikulilia ukaniponya.

Ee Bwana, usikie, unirehemu,
Bwana, uwe msaidizi wangu.
Uligeuza matanga yangu kuwa machezo;
Ulinivua gunia, ukanivika furaha.
Ee Bwana, Mungu wangu,
Nitakushukuru milele.
(K) Ee Bwana, Mungu wangu, Nalikulilia ukaniponya.

Somo la Pili
Ufu 5:1 1 -1 4
Mimi, Yohane, nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu, wakisema kwa sauti kuu, Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka. Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi ya juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia, vikisema, Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na milele. Na wale wenye uhai wanne wakasema, Amina. Na wale wazee wakaanguka, wakasujudu.

Shangilio
Lk 24:32
Aleluya, aleluya,
Bwana Yesu, utufunulie maandiko; Uwashe mioyo yetu unaposema nasi
Aleluya

Somo la Injili
Yn 21 :1 -1 9
Siku ile, Yesu alijidhihirisha tena kwa wanafunzi wake, penye bahari ya Tiberia, naye alijidhihirisha hivi. Simoni Petro, na Tomaso aitwaye Pacha, na Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, na wana wa Zebedayo, na wengine wawili wa wanafunzi wake, walikuwapo pamoja. Simoni Petro aliwaambia, Naenda kuvua samaki. Nao wakamwambia, Sisi nasi tutakwenda nawe. Basi wakaondoka, wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu. Hata asubuhi kulipokucha, Yesu alisimama ufuoni; walakini wanafunzi hawakujua ya kuwa ni Yesu. Basi Yesu akawaambia, Wanangu, mna kitoweo? Wakamjibu, La. Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki. Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini. Na hao wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila yapata dhiraa mia mbili; huku wakilikokota lile jarife lenye samaki. Basi waliposhuka pwani, wakaona huko moto wa makaa, na juu yake pametiwa samaki, na mkate. Yesu akawaambia, Leteni hapa baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi.
Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka. Yesu akawaambia, Njoni mfungue kinywa. Wala hakuna mtu katika wale wanafunzi aliyethubutu kumwuliza, U nani wewe? Wakijua ya kuwa ni Bwana. Yesu akaenda akautwaa mkate, akawapa, na samaki vivyo hivyo. Hiyo ndiyo mara ya tatu ya Yesu kuonekana na wanafunzi wake baada ya kufufuka katika wafu. Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia , Naam ,Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu. Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka. Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha kusema hayo akamwambia, Nifuate.

SEHEMU YA PILI: TAFAKARI
“NJONI MFUNGUE KINYWA”
Na, Pd. Nicas Mrosso, OFMCap

Yesu anatushibisha kwa neno lake na kwa Ekaristi Takatifu kisha anatutuma. Ndivyo anavyowaimarisha wanafunzi wake anapowatokea baada ya ufufuko wake.

Somo la I: Katika somo la Kwanza tunamwona Roho Mtakatifu anamjaza Petro na kumbadilisha yeye ambaye tutamsikia Yesu akimkabidhi mamlaka ya kuliongoza kanisa katika Injili. Yeye aliyekuwa akiogopa mamlaka za kiyahudi sasa anasimama mbele ya mahakama na makuu wa makuhani na kusema bila woga; “imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu”. Nasi ushuhuda wetu kwa ufufuko wa Yesu ni pale tunaposimama imara katika majaribu na vitisho.

Somo la II: Somo la Pili linatuingiza katika maono ya Yesu wa Ufufuko kama mwanakondoo aliyetukuzwa mbinguni. Tunapata matumaini ya kuwa imara na kuamnini kwamba ufufuko wa Yesu ndio mlango wa maisha ya umilele, maisha ya mbinguni. Kwa ufufuko wake tunapata uhakika wa milele mbinguni.

Injili: Tokeo la Yesu kwa wanafunzi wake mara ya tatu ni uthibitisho wa ufufuko wake kwa wanafunzi na kwetu. Hii inadhihirisha kwamba amefufuka kweli. Ndiye Bwana tunayemshangilia Pasaka. Yesu anadhihirisha kwamba ufufuko sio hadithi ya kutunga, sio roho kama ilivyo ya mizimu, na sio kama ufufuko wa Lazaro. Yesu Mfufuka anaishi, ni mzima, Yu hai mbinguni na duniani. Ndio maana anawafanyia muujiza wa kupata samaki, na baada ya muujiza huo anashiriki nao mlo/kifungwa kinywa na baadae anawatuma kupitia Petro kiongozi wa mitume na kanisa. Ishara ya samaki na Kuchunga kondoo ndizo kazi za kimisoari za kanisa.
Tunajifunza yafuatayo katika masomo ya leo;

Kusimama Imara katika Imani: somo la kwanza linatupa msisitizo huo. Kusipatikane kitu chochote cha kututenga na Kristo. Iwe mamlaka, iwe mila zetu, iwe kazi zetu, iwe changamoto, iwe matatizo ya maisha n.k. Yesu yeye anatuita daima ‘njoni mfungue kinywa.’

Tufungue macho yetu kumwona Yesu Mfufuka: Licha ya kwamba tumesherekea ushindi wa Yesu sikukuu ya Pasaka, bado tunaweza tukawa tumesharudi kwenye mazoea yetu ya mwanzo kama wanafunzi walivyorudia kazi yao ya kawaida ya uvuvi. Yesu anatualika kufungua macho yetu na kumwona katika mafanikio yetu. Wanafunzi waliporudi tena kuvua samaki hawakufanikiwa bila Yesu. Nasi tunachokifanya bila Yesu hakitafanikiwa. Na katika jambo lolote, lazima tusema, nimeweza hili katika yeye anitiaye nguvu. Ndio kusema “Ndiye Bwana” Kutambua uwepo wa Yesu katika Maisha yetu. Yeye ndiye anayebariki mafanikio yetu, ndiye anayebariki ushindi wetu, kufaulu kwetu, kupandishwa kwetu cheo, kuajiriwa kwetu, kufaulu kwetu, kuvuna kwetu, kujenga kwetu, kupona kwetu n.k

Tunakutana na Yesu Katika Karamu yake/Ekaristi Takatifu: Mwaliko uliowafanya wanafunzi wamtambue ni katika mlo, katika kifungua kinywa. Yesu mfufuka tunakutana nae katika Ekaristi Takatifu. Hii ndio namna ambayo Yesu amejifunua kwa wanafunzi wake, hata alipokuwa njiani na wanafunzi wa Emau (Lk 24:3 0-32). Ndio mwaliko wake kwetu ‘njooni mfungue kinywa’. Ndio mwaliko wa kumtambua katika Ekaristi Takatifu. Yeye mwenyewe alisema “Mimi ndimi chakula chenye uzima…na chakula nitoacho mimi ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Ewe ndugu yangu usikubali kukosa chakula hiki.

Umisionari/utume: Na baada ya kumtambua Yesu katika karamu, anatutuma kuwachunga kondoo wake. Petro, kiongozi wa mitume, anahojiwa mara tatu kama alivyomkana Yesu mara tatu, na Yesu anamtuma. Nasi baada ya kumpokea Yesu katika Ekaristi tunaulizwa mara tatu na Yesu, Je? Wanipenda? Ishi ukristo wako kiaminifu, kuwa mwanga kwa kondoo wangu, kuwa mwanga kwa wengine. Samaki na kuchunga kondoo ndiyo ishara ya kazi ya kitume ya Kanisa tunayopewa sisi kwa ubatizo wetu kupitia Petro Vika wa Yesu aliyekabidhiwa kanisa.

Tumwombe Mungu atujalie kumtambua Yesu katika maisha yetu na hasa tunapokutana nae katika karamu yake, na kupokea utume wake kwa kuwajibika kwetu kwa Imani yetu kwa Kanisa lake. Daima Yesu hatutumi tukiwa na njaa. Anatuita kwanza, ‘njooni mfungue Kinywa’ kisha anatutuma.

Bwana Awape Amani!

Kurudi kwa Tafakari Zote