Maungamo Matatu ya Kifransisko

Mwandishi: Datius Tumuombe


Aprili 10, 2025

UTANGULIZI
Neno “Maungamo” ni neno linalotumika sana katika mantiki za toba au kukiri dhambi lakini pia likimaanisha hali ya kukubali au kusadiki. Kadiri ya lilivyotumika kwenye Makala hii fupi ni kwa maana ya pili ya kukubali au kukubaliana. Kwa utajiri wake, hakuna "teolojia moja" ya kifransisko kwasababu ndugu mbalimbali wanafalsafa na wanateolojia wamechangia mawazo makuu katika historia ya Ufransisko lakini hatahivyo, kuna mambo yanabaki msingi kwa ujumla katika hali ya kiroho na teolojia kwa ujumla. Mambo hayo yanayobaki “msingi” ndiyo ninayoandikia hapa kama “Maungamo matatu ya Kifransisko.”

KUKUTANA NA KRISTO ALIYETWAA MWILI
Katika Makala ya mama Msekulari na mwandishi wa Kifransisko, Gabriele Uhlein, yenye kichwa: "Kukutana na Kristo Aliyetwaa Mwili: Uzoefu wa Kuishi Kristolojia;" Gabriele anaandika akigusia uandishi wa msomi wa Kibonaventura, Zachary Hayes, kwamba,

"Mtazamo wa Kifransiskani ... ni:
1. Umuhimu wa Kristo kama kiini,
2. Mungu kama Baba mwenye upendo, na
3. Uumbaji kama kioo na taswira ya Mungu.
Hayes anaeleza kuwa haya ndiyo maungamo matatu ambayo yaliendelezwa kuwa mitazamo ya kipekee ya kiteolojia na waanzilishi wa Shirika. Anaongeza pia kuwa Fransisko alieleza 'imani' hizi kwa namna yake binafsi, vivyo hivyo na Clara. Ningeweza kuongeza kuwa ili tafakari yoyote ya kiteolojia iitwe ya Kifransiskani, ni lazima iunge mkono mambo hayo matatu. Jukumu langu basi ni kueleza maarifa hayo kwa namna inayofaa na inayoendana na hali halisi ya dunia ninayoiona. Nitajaribu kufanya hivyo hapa. Lakini kuna onyo—kuyaeleza kwa namna inayobadilisha maisha daima, kwa roho ya Husia wa Tano kama alivyopendekeza Hayes: “Jitahidi kutambua heshima ambayo Mungu amekupa. Alikuumba na akaufanya mwili wako kwa mfano wa Mwanae mpendwa, na nafsi yako kwa sura Yake.” (Hayes, The Cord, 46.1 (Jan./Feb.,1996): 3-17)."

Mambo matatu yaliyotajwa ndiyo maungamo yanayoelezwa hapa. Tutaona kiini cha kila ungamo walau kwa ufupi.

1. UMUHIMU WA KRISTO KAMA KIINI
“Ukatikati” wa Kristo au Kristo kama Kiini ni dhima kuu ya teolojia wa Kifransiskani na Wafransisko wengi wamendika sana juu ya dhima hii kwa mfano mwandishi maarufu, Richard Rohr, OFM, ambaye katika vitabu vyake Zaidi ya 30, kitabu cha The Universal Christ aliona kiwe ufupisho wa uandishi wake wote alipoamua kumpelekea Papa Fransisko kama zawadi miaka ya hivi karibuni. Fransisko wa Asizi ndiye baba ya teolojia hii ingwaje hakuwa “msomi.” Fransisko aliwaita viumbe wote kaka na dada kwasababu ya Umwilishio wa Kristo unaoonekana katika uumbaji wote. Fransisko anasema katika Wosia kwamba, “Jukumu langu ni kuwa mdogo wa watu wote ulimwenguni, sio tu kwa wanadamu bali hata kwa wanyama wote” (SalVirt 16-18). Juu ya maneno hayo ya Wosia, dada Gabriele anaongeza kwa kusema, “Mateso yangu na kusulubiwa kwangu ni mambo yasiyoepukika katika kumbatio hilo, lakini vivyo hivyo ni ufufuo wangu na ukamilifu wa maisha yangu. Kuhusu haya, tuna hakikisho la Neno ambaye alifanyika mwili." (The Cord, 48.2 (1998, 50-62).

2. MUNGU KAMA BABA MWENYE UPENDO
Picha ya Mungu kama Baba imekumbwa na kutoeleweka vizuri kwasababu ya donda baba katika jamii kwa sehemu kubwa. Baba ni mtu ambaye daima hayupo nyumbani na kwa ujumla, “mlevi.” Picha imefanya jamii kama vile za ulaya na Marekani kuanza kutumia kiwakilishi cha junsia ya kike kwa Mungu. Hata hivyo, ni ungamo la Wafransiskani kumuonesha Mungu kama Baba mwenye Upendo. Akitambua changamoto hii kwa jamii yake, dada msekulari, Gabriele Urlein anamnukuu Sara Ruddick katika kitabu chake, Maternal Thinking: Towards a Politics of Peace, anapoeleza sifa ambazo zinafafanua utendaji wa Mungu kama Baba mwenye huruma:

i). Hushikilia kwa karibu, anakubali mabadiliko. Hii ni uwezo wa kuendelea kuwa katika uhusiano wa upendo kadri mtoto anavyokua. Mabadiliko yanayoashiria ukuaji wa mtoto kuelekea ukomavu wa ubunifu ni jambo la kusherehekewa na si la kujutia. Hakuna jaribio la kuzuia mchakato wa mabadiliko. Mabadiliko yanakaribishwa kwa sababu yanaendelea kufunua uwepo wa Mungu—mchakato wa kuendelea kupanuka kwa uzoefu wa uwezekano wa "Mungu pamoja nasi."

Andiko la Biblia:
“Kwa maana mimi najua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa tumaini siku zenu za mwisho.”
— Yeremia 29:11

ii). Hutazama kwa makini kilicho cha kipekee badala ya kile cha jumla na kisichoeleweka. Kila mtoto anapendwa kwa upekee wake binafsi. Wazo la kuwapenda watoto wote kwa usawa halionekani katika kuwafanyia mambo kwa njia sawa, bali linajidhihirisha kupitia majibu makini na ya kibinafsi kulingana na mahitaji na maslahi bora ya kila mtoto. Kila mmoja wetu, na kila kipande cha uumbaji, kinapendwa kwa upekee usiorudiwa tena wa upendo wa kimungu. Anathamini historia yake ya kipekee iliyoonyeshwa katika mwili wa binadamu uliogharimu sana.

Andiko la Biblia:
“Naam, nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope; ninyimwafaa zaidi kuliko mashomoro wengi.”
— Luka 12:7

iii). Hakuna hata mmoja wetu aliye na uzoefu sawa wa furaha wala anayeishi mahali pamoja katika muda na nafasi. Na kila mmoja wetu, kulingana na maisha yake ya kipekee, amehisi gharama ya kuishi katika mwili. Hakika, kuishi katika mwili kuna gharama. Miili yetu inahitaji matunzo, huhisi maumivu, hupata magonjwa, hudhoofika, na hatimaye hututoka. Kujua hili ni kuwa na uwezo wa huruma kuu na upendo wa busara. Je, si uso wa Kristo unatusindikiza hata huko pia?

Andiko la Biblia:
“Kwa kuwa hamna Kuhani Mkuu asiyeweza kushiriki nasi katika udhaifu wetu, bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.”
— Waebrania 4:15

iv). Hutambua upendekano na hutoa upendo ambao “ujuzi” hauuangamizi. Kuna uwezo fulani wa kupenda ambao haupungui hata mbele ya ukweli. Haijalishi watoto wanaweza kufanya nini, haijalishi matokeo ya tabia yao, upendo uliopo kwao hubaki thabiti, na hata unaweza kuendelea kukua. Kujua yaliyopita, hata yale yasiyopendeza, na upendo wa Mungu kuendelea licha ya hayo, ndilo tumaini la kweli la kila mwenye kutubu.

Andiko la Biblia:
“Lakini Mungu aonyesha pendo lake kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu tulipokuwa tungali wenye dhambi.”
— Warumi 5:8

3. UUMBAJI KAMA KIOO NA TASWIRA YA MUNGU
Richard Rohr, OFM, anasema uumbaji wote ni mahali pa kujificha na kujifunua kwa Mungu. Hii inaonekana katika maandishi Mt. Bonaventura anapoeleza kuhusu uumbaji kwamba kwa Yesu kiugeuka sura, uumbaji nao uligeuka sura kwani uumbaji umetokana na Kristo kama Paulo anavyoandika, “Pasipo yeye hakuna kilichofanyika” (Yohane 1:3). Mt. Bonaventura anaandika:

Vitu vyote husemwa kuwa vimebadilishwa katika kugeuka sura kwa Kristo, kwa kadiri ambavyo kuna kitu katika kila kiumbe kilichobadilishwa ndani ya Kristo. Kwa kuwa kama mwanadamu, Kristo anashiriki jambo fulani na viumbe vyote. Na jiwe anashiriki kuwepo; na mimea anashiriki uhai; na wanyama anashiriki hisia; na malaika anashiriki akili. Kwa hiyo, vitu vyote husemwa kuwa vimebadilishwa ndani ya Kristo kwa sababu katika asili yake ya kibinadamu alijumuisha ndani yake kitu kutoka kwa kila kiumbe alipogeuka sura. (Bonaventura, Sermo I, Dom II in Quad. IX, 215-219).

Uumbaji wote, kwa kugeuka sura kwa Yesu (kadiri ya Mt. Bonaventura) lakini hata kwa kuwa tu viumbe wa Mungu (kadiri ya Mt. Fransisko wa Asizi), ni kioo ambamo tunamuona Mungu na ni taswira ya Mungu vilevile. Ndio maana Yesu anasema na kusisitiza upendo kwa jirani ana hata adui kwakuwa uumbaji wote ni kioo na taswira ya Mungu.

HITIMISHO
Maungamo matatu ya Kifransisko ni uroto wa kinachoweza kuitwa spirituality au hasa, teolojia ya Kifransiskani. Kama Wafransisko tunaujumbe kwa ulimwengu juu ya ukiini wa nafasi ya Kristo (the centrality of the figure of Christ), Mungu kama Baba mwenye upendo (God as the Loving Father), na Uumbaji kama kioo na taswira ya Mungu. Haya hutuunganisha na kuupa mwangwi usiokoma ujumbe wa Mt. Fransisko na Wafuasi wake kwa nyakati zote. Amani na Salama!

Rudi kwenye Orodha