Juhudi Gani Zinafanywa na Wafransiskani Kuhusu Mazingira?

Mwandishi: Datius Tumuombe


Aprili 05, 2025.

UTANGULIZI
Siku ya Jumapili ya Pasaka ya mwaka 1980, Papa Yohane Paulo II alimtangaza Fransisko wa Asizi kuwa msimamizi (au mlinzi) wa "ikolojia" au kwa lugha rahisi zaidi: Mazingira na viumbe vilivyomo. Mt. Yohane Paulo II bila shaka alimuona Mt. Fransisko wa Asizi na Wafransiskani kwa ujumla kama “chumvi” ya ulimwengu katika kubadili umakini yaani “focus” kutoka kwa binadamu tu, kwenda kwa viumbe wengine pia. Katika mwaka huu wa Matumaini, ni nafasi ya kutafakari tena nafasi ya Wafransiskani katika kuleta tumaini kwa uumbaji wote tukiangaza na kuchangamotisha juhudi zinazofanywa na Wafransiskiani kuhusu mazingira.

MADA YENYEWE
Mada hii ni kichocheo nilichokipata kutoka Makala ya Nd. Keith Warner, OFM, katika Jarida la The Cord, ambapo anajiuliza maswali mbalimbali hasa kuhusu nafasi ya Wafransiskani katika Ikolojia. Anajiuliza maswali kama:

Swali: Watawa wa Kifransisko wapo wapi katika mjadala kuhusu mazingira?
Swali: Ni juhudi gani zinafanywa kushughulikia masuala ya mazingira kwa mtazamo wa Kifransisko?
Swali: Je, familia ya Kifransisko ina mchango wa kipekee wa kutoa? Kama wafuasi wa mtakatifu mlinzi wa ikolojia, tunayo dhamana ya kutenga angalau sehemu ya juhudi za maisha yetu kuiga mfano wake wa upendo kwa uumbaji. Tunawezaje kufanya hivi? (The Cord, 48.2 (1998), 74.)

Maswali haya ni muhimu kwetu pia leo hasa tunapoadhimisha miaka 45 tangu baba yetu Mt. Fransisko afanywe mlinzi wa Ikolojia. Swali msingi linabaki: Sisi je tunafanya juhudi gani kuhusu mazingira?

LAUDATO SI
Kusema Papa Fransisko ni Fransisko wa pili ni changamoto kwa Wafransiskani waliokuwepo tangu enzi wa Fransisko mwenyewe, tangu kare ya 13 lakini kuna ukweli katika changamoto hii hasa linapokuja suala la mazingira. Kumewahi kuwepo na mapapa Wafarnsiskani walau kina Papa Nicholas IV (1288-1292), Sixtus IV (1471-1484) na Clement XIV (1769-1774). Pamoja na hao, hakuna papa katika historia aliyewahi kuandika waraka wa kipapa akiutoleo wote kutetea uumbaji, ukurasa wa kwanza mpaka wa mwisho. Papa Frasisko amefanya tofauti. Ndio, yapo mapungufu na hata kwamba sio mfransisko bali ni mjezuiti, lakini kwa Laudato Si alitoa changamoto.
Kwa asili, Laudato Si ni wimbo wa Viumbe uliotungwa na Mt. Fransisko na unasemekana kuwa kazi ya kwanza ya ushairi kuandikwa kwa kiitaliano. Fransisko anataja viumbe vyote kama kaka na dada tangu kaka Jua hadi dada mauti. Ni kazi ya Sanaa na sala inayomsifu na kumtukuza Mungu katika uumbaji wake. Mimi na wewe tunaweza kujiuliza, “Tumefanya nini katika kumsifu Mungu katika uumbaji wake?” “Ni kwa namna gani tumeishika amri ya kwanza katika kitabu cha Mwanzo (1:28) kama watunzaji wa kazi ya Mungu?

MIKAKATI PENDEKEZWA
Katika ulimwengu wa leo ambako mazingira yanakumbwa na changamoto nyingi — kama mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira, na uharibifu wa bioanuwai — tunanafasi ya kipekee ya kama Ndugu Wafransisko ya kuwa mashahidi wa matumaini na wapatanishi wa uumbaji. Kwa kuzingatia roho ya Mtakatifu Fransisko wa Asizi, ambaye aliona viumbe wote kama ndugu, mikakati kadhaa ifuatayo yaweza kufaa:

1. Kujenga Uelewa wa Kiroho wa Uumbaji
Wafransisko, kwa mfano wa Papa Fransisko wa Laudato Si, tuandae mafundisho na tafakari zinazojikita katika roho ya uumbaji — kuelewa kwamba dunia ni zawadi kutoka kwa Mungu, si mali ya binadamu. Hii inaweza kujumuisha tafakari za mfano wa Mtakatifu Fransisko wa Asizi alivyohusiana na viumbe.

2. Kuishi maisha ya Udogo na Yanayoheshimu Mazingira
Hii ni pamoja na kutumia rasilimali kwa uangalifu, kupunguza matumizi ya plastiki, nishati, na kula vyakula vinavyozalishwa kwa njia endelevu. Kwa mfano, mashirika ya kifransisko yanaweza kuanzisha bustani endelevu au kutumia nishati jadidifu.

3. Elimu na Ushawishi kwa Jamii
Wafransisko tuwe mstari wa mbele katika kutoa elimu kuhusu utunzaji wa mazingira, hasa kwa vijana na watoto. Hii inaweza kufanyika kupitia warsha, semina, au hata njia za kisasa kama mitandao ya kijamii. Pia waweke mkazo katika kushawishi sera zinazolinda mazingira.

4. Kuonyesha Ushirika na Viumbe Vyote
Kama alivyo Mt. Fransisko, wafuate moyo wa undugu na viumbe vyote: binadamu, wanyama, mimea, na mazingira kwa ujumla. Hili linaweza kuonyeshwa kwa kuanzisha huduma kwa wanyama waliotelekezwa, upandaji miti, kulisha ndege kwa kuwatengea chakula kigogo sehemu Fulani wanayoweza kufika na shughuli za kijamii za “kijani.”

5. Sala na Tafakari kwa Ajili ya Uumbaji
Kuwe na utaratibu wa sala maalum kwa ajili ya uumbaji, hasa katika kipindi cha Season of Creation (Septemba 1 – Oktoba 4). Sala hizi ziwe na tafakari juu ya nafasi ya mwanadamu katika dunia na hitaji la toba kutokana na uharibifu wa mazingira.

HITIMISHO
Mada hii yenye kichwa mtindo wa swali imelenga kuchangamotisha nafasi wa Wafransiskani katika ulimwengu wa leo kwa nafasi yao ya dhamana kwa ikolojia. Tumeona sio tu changamoto kwa Wafransiskani kutokana na Laudato Si, bali pia mikakati pendekezwa. Ni hekima pia kukiri kwamba wapo Wafransiskani wengi wanaofanya juhudi kuhusu mazingira lakini pengine bila motisha. Yafaa sasa kuwapa ndugu hao motisha na kila mmoja wetu kuona nafasi yake inavyohitajika sana katika kumtukuza Mungu kwanjia ya uumbaji. Amani na Salama!

Rudi kwenye Orodha