Madonna Poverta

Mwandishi: Datius Tumuombe


22 Machi, 2025

UTANGULIZI
“Madonna Poverta,” au kwa Kiswahili Bibi Ufukara ni dhana aliyopenda kutumia Mt. Fransisko (1181–1226) kueleza hali ya kujinyima mali ya kidunia kwa ajili ya kumfuata Kristo. Makala hii fupi itajikita katika kuangazia “ukatikati” wa dhana hii katika maisha ya Mt. Fansisko wa Asizi kama ambavyo wandishi mbalimbali kama Efrem Trettel anaeeleza kwamba, Fransisko alifuata “ufukara,” “Madonna Poverta” kwa utii wa ndani wa mfuasi.

DHANA YA MADONNA POVERTA
Kwa Fransisko Madonna Poverta ilitumika kuonesha uhusiano wake wa kiroho na wito wake wa kuishi maisha ya unyenyekevu na umaskini wa hiari. Ndani ya maandiko kama vile The Sacrum Commercium (Kwa Kiingereza: The Holy Commerce of St. Francis with Lady Poverty), dhana ya Madonna Poverta inatajwa mara nyingi, ikiwa ni mfano wa ndoa ya kiroho kati ya Fransisko na maisha ya unyenyekevu. Katika mafundisho yake kwa wafuasi wake, Fransisko aliwahimiza pia kuishi kwa kumkumbatia Madonna Poverta.
Katika tafakari za Fransisko, Madonna Poverta kumbe iliwakilisha ufukara kama bibi-arusi wa roho ya mtu. Fransisko aliona ufukara si kama hali ya kukosa bali kama chaguo la hiari la kuachana na mali ili kupata utajiri wa kiroho. Kwa Fransisko, kuwa maskini kulimaanisha kujiweka huru dhidi ya tamaa za dunia na kuishi kwa kutegemea neema ya Mungu pekee.

MAISHA YA FRANSISKO WA ASIZI NA "MADONNA POVERTA"
Mtakatifu Fransisko alizaliwa katika familia tajiri ya wafanyabiashara lakini aliamua kuacha mali zote baada ya kupata wito wa kiroho. Alivaa mavazi mepesi, akakataa anasa, na kuanza kuishi maisha ya ufukara yaani umaskini wa kujitolea. Alijitambulisha na maskini, wagonjwa, na wanyonge wa jamii, akiwahudumia wote kwa upendo.
Fransisko aliamini kwamba kwa kumkumbatia Madonna Poverta, alikumbatia Yesu Kristo aliyekuwa fukara. Hili lilimwongoza kuanzisha Shirika baada ya kuwa wafuasi kadhaa wameanza kuandamana naye na kwa akili ya “Madonna Poverta,” alitaka wafuasi wake waitwe Ndugu Wadogo, kama ilivyo mwishoni mwa majina yao. Kwa Wakapuchini ni Ndugu Wadogo Wakapuchini, kwa Wakonventuali na “Wafransiskiani,” wote wanatumia Ndugu Wadogo au OFM katika majina yao.

CHANGAMOTO ZA KUMKUMBATIA MADONNA POVERTA KWA NYAKATI HIZI
Kumkumbatia Madonna Poverta kunakabiliwa na changamoto nyingi katika dunia ya sasa hasa kwetu vijana. Mwelekeo wa jamii kuelekea utajiri na mafanikio ya kifedha hufanya watu wanaoishi maisha ya kujinyima kuonekana kana kwamba wanakwepa maendeleo au wanafanya maamuzi yasiyoeleweka. Matumizi ya anasa mara nyingi huhusishwa na heshima na hadhi, jambo linalofanya kumkumbatia Madonna Poverta ionekane kama udhaifu.
Gharama za maisha zinapoongezeka, watu wengi wanakabiliwa na changamoto za kukidhi mahitaji yao ya msingi. Kumkumbatia Madonna Poverta inahitaji maamuzi magumu, hasa kwa wale walio na familia au wanaowategemea. Shinikizo la kiuchumi na ukosefu wa uhakika wa kifedha vinaweza kufanya maisha haya yawe magumu zaidi.
Pia teknolojia na mitandao ya kijamii pia hasa katika zama zetu za Akili Bandia maarufu kama AI, zinachochea tamaa ya kumiliki vitu zaidi kwa kuonyesha mtindo wa maisha wa kifahari na mafanikio ya kifedha. Hali hii inawafanya watu wengi kuhisi kuwa wanahitaji kumiliki zaidi ili kufanikisha maisha bora. Katika mazingira haya, kumkumbatia Madonna Poverta kunaweza kuhisi kama kujitenga au kupingana na maadili ya kisasa.
Changamoto nyingine ni ya kisaikolojia na kihisia. Kumkumbatia Madonna Poverta kunaweza kusababisha hisia za upweke au kutoeleweka na jamii. Bila msaada wa kijamii au wa kiroho, watu wanaochagua njia hii wanaweza kuhisi kutengwa. Zaidi ya hayo, mgongano wa wajibu wa kifamilia na maadili ya unyenyekevu unaweza kufanya uamuzi wa kuishi maisha haya kuwa mgumu zaidi.

NENO LA FARAJA KUTOKA KWA MT. FRANSISKO
Fransisko aliwafariji ndugu kwa nadhiri walizoweka kwa Mungu kwamba “Makubwa tumeahidi, makubwa zaidi tumeahidiwa.” Katika Maandishi ya Fransisko pia, mpangiliaji wa maandishi hayo kwenye “Omnibus” anaweka maneno haya:
Ishi daima katika ukweli
Ili kwamba ufe katika utii.
Usisumbuke na maisha ya nje
Kwani yale ya kiroho ni bora.
Fransisko mara nyingi alimsifu Madonna Poverta kama mama wa fadhila zote. Aliandika mashairi na sala yaliyomsifu bibi ufukara kama njia takatifu ya maisha. Hasa, katika “Wimbo wa Ndugu Jua,” alionesha shukrani kwa kila zawadi ya uumbaji huku akidumisha roho ya unyenyekevu.

HITIMISHO
Kwa Mtakatifu Fransisko wa Asizi, Madonna Poverta haikuwa hali ya kukosa mali bali hasa njia ya kuelewa fumbo la msalaba na upendo wa Kristo. Leo, mfano wake unaendelea kuwahamasisha watu wengi kuishi kwa unyenyekevu, kusaidia wahitaji, na kujikita katika maisha ya kiroho. Madonna Poverta kumbe haibaki kuwa dhana, bali mwaliko wa kweli wa kumfuata Kristo kwa moyo safi na mnyenyekevu.

Rudi kwenye Orodha